
Vijana
wametakiwa kuacha kuwa watazamaji wa fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali
badala yake watumie fursa hiyo kuwekeza kupitia fedha za mkopo zinazotolewa na
serikali kuanzisha miradi itakayowakwamua kiuchumi.
Rai hiyo
imetolewa na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais maendeleo ya vijana Dkt. Joel Nanauka wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la vijana Mkoa wa
Shinyanga,ambapo amewataka vijana
kuwekeza kwenye muda na kuchangamkia fursa bila kusubiri kuonewa huruma.
Amesema kufanikiwa kunatokana na ndoto
ulizonazo,ikiwa ni pamoja na kuwa na nidhamu ya muda hatua ambayo itawafikisha kwenye
mafanikio badala ya kuendelea kulalamika bila kuchukuwa hatua ili kuondokana na
umasikini.
“ Vijana
tumieni fursa kupitia fedha zilizotolewa
na serikali Sh 200 bilioni kuandika maandiko ya miradi ambayo italenga
kuanzisha jambo ambalo litaleta tija na kuweza kuwasaidia vijana”amesema
Nanauka.
Amesema
serikali imeondoa masharti magumu yaliyokuwa kikwazo kwa vijana kunufaika na
mikopo, likiwamo sharti la dhamana isiyohamishika, ili kuwawezesha vijana wengi
zaidi kupata fedha za uwezeshaji Sh bilioni 200 zilizotolewa na Rais Samia
Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana.
Nanauka
amesema masharti yaliyokuwa yanawakwamisha vijana wengi kupata mikopo sasa
yamefutwa, ikiwamo dhamana isiyohamishika, huku marejesho yakianza kati ya
miezi mitatu hadi sita baada ya kupokea mkopo, ili kuwapa muda wa kukuza miradi
yao.